Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mji wa Geita Modest Apolinary, kupisha uchunguzi kufuatia ununuzi wa gari yenye dhamani ya shilingi millioni 400.
Waziri Jafo amesema kuwa mara baada ya Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baraza la Madiwani kuvunjwa majukumu yote yalisimishwa kwa wakurugenzi na kupelekea baadhi ya Halmashauri kutumia muanya huo kufanya ubadhilifu wa fedha za umma.
“Halmashauri ya Mji wa Geita, katika kipindi hicho ambacho baraza la madiwani halipo waliweza kununua gari lenye dhamani ya shilingi milioni 400, jambo hili halikubaliki kwa kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma”amesema Waziri Jafo
Waziri Jafo amemuagiza Katibu Mkuu wa TAMISEMI Mhandisi Nyamhanga, kuunda timu ya uchunguzi ambayo itachunguza kwa kina matumizi ya fedha katika Halmashauri ya mji Geita.
Sambamba na hilo amekiagiza kitengo cha ukaguzi Ofisi ya Rais-TAMISEMI kufanya uchunguzi na ufuatiliaji kwa Halmashauri nyingine zenye kutiliwa shaka kama zilienda kinyume cha taratibu ya matumizi ya fedha.