Afisa Habari wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Ally Kamwe anaamini kikosi chao kitarejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu baada ya mchezo wa Oktoba 23.

Young Africans jana Jumatatu (Oktoba 03) ilifikisha alama 10, baada ya kuchomoza na ushindi wa 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting na kujikuta ikikwama nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, huku Simba SC ikiwa kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufungwa na kufunga.

Ally Kamwe amesema ushindi dhidi ya Maafande wa Ruvu Shooting ni hatua kubwa sana kwa Young Africans katika harakati za kutaka kurejea kileleni mwa msimamo, hivyo mchezo ujao dhidi ya Simba SC anaamini mambo yatawanyookea na kuvuna alama tatu zitakazowawezesha kufikisha alama 16.

“Alama tatu tulizopata baada ya ushindi wetu dhidi ya Ruvu Shooting jana Jumatatu, zinatuweka mahali pazuri kwenye msimamo wa Ligi, huyo atakaeondoka akiamini anaongoza Ligi alama za kutupisha zipo kwake. Kwa hiyo ni suala la muda tu.” amesema Ally Kamwe

Young Africans inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Simba SC Oktoba 23 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao utapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Siku za karibuni Simba SC imekua ikiambulia matokeo mabaya dhidi ya Young Africans, ikipoteza mara mbili mfululizo, awali ilikubali kufungwa 1-0 jijini Mwanza, Uwanja wa CCM Kirumba kwenye mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na mwanzoni mwa msimu huu ilikubali kufungwa 2-1 katika mpambano wa Ngao ya Hisani uliounguruma Uwanja wa Mkapa.

Upande wa Michezo ya Ligi Kuu msimu uliopita 2021/22, Manguli hao wa Soka la Bongo walitoshana nguvu kwa kutoka suluhu kwenye michezo yote miwili.

TANESCO kunufaika ujenzi wa kinu cha kupoza umeme GGML
Geita Gold FC yavuna ushindi wa kwanza 2022/23