Uongozi wa Young Africans ni kama umempa maagizo mazito kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamond baada ya kusema kwa kuwa msimu uliopita walifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, basi msimu huu hakuna kinachoshindikana kufikia malengo yao.
Young Africans msimu uliopita walicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Algers ambapo walipoteza kwa faida ya bao la ugenini.
Msimu huu mpaka sasa wapo katika Mzunguuko wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika, wakienda kucheza dhidi ya Al Merrikh ya Sudan kuwania kutinga hatua ya makundi.
Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema: “Kila shabiki wa Young Africans na Afrika nzima wanafahamu msimu uliopita Young Africans tulicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo hiyo ni meseji nzito kwa Kocha Gamondi na wachezaji wapya wa Young Africans wafahamu timu haitakuwa tayari kushindwa kufika mbali.
“Kocha tayari anafahamu kuwa msimu uliopita Young Africans tulicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, hii meseji kubwa sana kwake na inakuwa kama agizo la Young Africans msimu huu kufika mbali zaidi katika michuano hii ya kimataifa ambayo tunashiriki.
“Wachezaji wageni pia wanapata ujumbe wao juu ya jambo hili kwamba Young Africans inatakiwa kufika mbali kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita.
Tayari malengo yetu msimu huu ni kuona tunafika hatua ya makundi na tukifanikiwa kumfunga AI Marrikh safari yetu itakuwa nzuri zaidi.”