Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans umeweka wazi kuwa kazi ipo msimu mpya wa 2023/24 kutokana na mipango makini inayosukwa kwenye klabu hiyo.
Young Africans ni mabingwa watetezi wa ligi baada ya kukamilisha msimu wakiwa washindi wa kwanza, pia walibeba Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
Timu hiyo imeshakamilisha utambulisho wa wachezaji wao ikiwa ni pamoja na Gift Fred kutoka SC Villa ya Uganda, Jonas Mkude aliyekuwa Simba, Nickson Kibabage kutoka Singida Fountain Gate, Maxi Nzengeli alikuwa anakipiga Maniema FC na Yao Attohoula kutoka ASEC Mimosas.
Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema kuwa kazi kubwa itakuwepo msimu ujao kutoka kwa wachezaji wa timu hiyo kutimiza majukumu yao.
“Kazi kubwa ipo kwa msimu ujao na tunaamini tupo tayari kwa ajili ya ushindani kwa kuwa maandalizi yanaendelea na ambacho tutakifanya ni kuendelea pale ambapo tuliishia.
“Mashabiki wanapenda kuona timu ikipata ushindi nasi tunahitaji kufanya hivyo kutokana na ukweli kuwa ili ushinde ni lazima uwe na maandalizi mazuri hilo tupalifanya kwa umakini,” amesema Kamwe.