Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wametamba kiufumua US Monastir ya Tunisia katika mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Young Africans ndio wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika Barani Afrika, ambapo wanatarajiwa kushuka Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam keshokutwa Jumapili (Machi 19), kuanzia saa moja usiku.
Afisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe ameweka wazi kuwa tayari wamewasoma wapinzani wao na wamekamilisha asilimia zaidi ya 90 ya hesabu za maandalizi yao na kuchimba mkwara ni lazima wataibuka na ushindi.
Kamwe amesema: “Tunaendelea na taratibu mbalimbali za hamasa kuelekea mchezo wetu dhidi ya US Monastir, mpaka sasa tumekamilisha zaidi ya asilimia 90 a maandalizi yetu tunajua utakuwa mchezo mgumu lakini tuna uhakika wa ushindi.”
“Tumewasoma wapinzani wetu na tunajua ubora na mapungufu yao, hivyo licha ya kuutarajia mchezo mgumu lakini tuko tayari na tuna ari ya kuandika historia ya kucheza robo fainali baada ya muda mrefu kupita.”
Katika msimamo wa kundi D la mashindano hayo Young Africans mpaka sasa wamefikisha alama 07 na kuendelea kubaki nafasi ya pili, hivyo kama watashinda mchezo wa Jumapili (Machi 18) watafuzu Robo Fainali kwa mara ya kwanza.