Mlinda Lango chaguo la Tatu katika kikosi cha Simba SC Ally Salim, amesema kuwa juhudi na ushirikiano ni sababu iliyomfanya afanikiwe kufanya vizuri katika mchezo dhidi ya Young Africans, uliopigwa juzi Jumapili (April 16), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Ally Salim alicheza kwa mara ya kwanza mchezo wa Kariakoo Dabi, na kufanikiwa kuiwezesha Simba SC kutoka uwanjani kibabe kwa kuibanjua Young Africans mabao 2-0.
Mlinda Lango huyo aliokoa michomo ya Fiston Mayele, Tuisila Kisinda na Bernard Morrison ambao walikuwa kwenye ubora wao.
Hata hivyo ulikuwa mchezo wa pili kwa Salim kukaa langoni msimu wa 2022/23 kunako Ligi Kuu Bara baada ya awali kucheza dhidi ya lhefu FC, mchezo uliochezwa Uwanja wa Highland Estate, mkoani Mbeya na Simba SC ilichomoza na ushindi wa 0-2.
Akizungumzia mafanikio ya kukaa langoni pasina kuruhusu bao katika mchezo dhidi ya Young Africans Salim amesema: “Ni furaha kwetu kushinda na tunatambua haikuwa kazi rahisi, iliwezekana kutokana na ushirikiano ambao wachezaji tumeufanya kwa kila mmoja kutimiza majukumu yake.”
“Tunamshukuru Mungu kwa kupata ushindi kwa kuwa ni kitu ambacho tulikuwa tunahitaji na tumefanikiwa kupata pointi tatu muhimu,” alisema kipa huyo ambaye alikaa langoni baada ya kipa namba moja, Aishi Manula kuumia, huku kipa namba mbili, Beno Kakolanya, akiishia benchi.
Katika mchezo huo wa Mzunguuko wa 26 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mabao ya Simba SC yalikwamishwa wavuni na Beki kutoka DR Congo Henock inonga Baka na Mshambuliaji wa Tanzania Kibu Denis Prosper.