Meneja wa klabu bingwa nchini Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG) Thomas Tuchel, amekiri kuridhishwa na kiwango cha mlinda mlango Alphonse Areola na kusema huenda akawa chaguo la kwanza na kumpiku mkongwe Gianluigi Buffon.
Tuchel amefikia hatua hiyo baada ya kumfuatilia mchezaji huyo katika michezo miwili ya timu ya taifa ya Ufaransa, ambayo ilishuhudiwa ikipambana dhidi ya Ujerumani na kuambulia matokeo ya sare ya bila kufungana na kisha Ubelgiji waliokubali kufungwa bao moja kwa sifuri.
Meneja huyo kutoka nchini Ujerumani amesema, Areola ana uwezo mkubwa na ameonyesha kujiamini kupitia michezo hiyo miwili aliyocheza, japo Buffon ana vitu adimu ambavyo vina uwezo wa kuinusuru timu katika mapambano magumu.
“Sijafanya maamuzi ya mwisho, hapa ninazungumzia uwezo wa Areola aliounyesha katika michezo miwili ya Ufaransa aliyopewa nafasi ya kukaa langoni, lolote linaweza kutokea,” Tuchel aliiambia RMC Sports.
“Areola amekuzwa na PSG na anajua mazingira ya klabu hii tangu akiwa na umri mdogo, amejifunza mambo mengi kupitia walinda mlango waliomtangulia na kuondoka, lakini naamini muda huu, huenda ukawa muda wake,” aliongeza.
Alisema kuwa Gianluigi Buffon ataendelea kuwa mlinda mlango mwenye uzoefu mkubwa katika soka la barani Ulaya na duniani kwa ujumla, na kwamba ukongwe wake unasaidia kwa namna fulani, hasa anapokuwa kwenye klabu kama PSG.
Hata hivyo, alienda mbali na kumtahadharisha ajiandae na changamoto mpya kutoka kwa Areola.
Mabingwa hao wa Ufaransa wanatarajia kurejea katika ligi ya nchini humo mwishoni mwa juma hili, na watapambana na Saint-Etienne, lakini bado haijafahamika nani ataanza langoni kati ya Areola ama Buffon.