Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema Serikali inathamini na kutambua mchango mkubwa wa taasisi za dini katika shughuli mbalimbali za maendeleo hususani katika kuimarisha amani na utulivu wa nchi.
Simbachawene, ametoa kauli hiyo alipomuwakilisha Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango kwenye hafla ya chakula cha hisani iliyoandaliwa kwa ajili ya kuchangia ukamilishaji wa ujenzi wa jumla wa Kanisa Katoliki la Parokia ya Utatu Mtakatifu Changanyikeni jijini Dar es Salaam.
Aidha, amewapongeza Wanaparokia hao kwa hatua kubwa waliyofikia katika ujenzi wa kanisa hilo huku akiwasihi kuendelea kuiunga mkono Serikali katika masuala ya maendeleo na kusema, “Hongereni sana kwa hatua hii kubwa mliyofikia ya umaliziaji wa Kanisa hili, hakika mmefanya kazi kubwa na nzuri.”
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Parokia ya Kanisa hilo, Gallen Mvungi jumla ya kiasi cha shilingi milioni 250 kinahitajika kukamilisha ujenzi wote ambapo shilingi milioni 50 tayari zimeshakusanywa na wanaparokia hiyo ambapo jumla ya kiasi cha shilingi milioni 110 zilikusanywa, shilingi milioni 78 zikiwa ni ahadi na milioni 32, fedha taslimu.