Kiungo Mshambulaiji wa klabu ya Young Africans Dickson Ambundo, ameahidi kupambana kadri atakavyoweza ili kufanikisha lengo la klabu hiyo kurejesha heshima ya kutwaa mataji kuanzia msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaoanza rasmi mwishoni mwa mwezi Septemba.
Ambundo aliyejiunga na Young Africans mwezi Agosti akitokea Dodoma Jiji FC, amesema kusajiliwa kwake klabuni hapo ni sehemu ya kufanikisha lengo la kutwaa mataji, hivyo hana budi kujitayarisha kwa mapambano ambayo anaamini yataleta tija mwishoni mwa msimu 2021/22.
Kiungo huyo amesema, Young Africans ni klabu kubwa na inapaswa kuwa kwenye hadhi ya kutwaa mataji makubwa ya ndani na nje ya nchi, hivyo baada ya jambo hilo kuwa changamoto kwa muda mrefu, anaamini muda wa kurejesha furaha kwa Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hata hivyo Ambundo amesema kazi hiyo hatoifanya pekee yake, bali wachezaji wote wanaounda kikosi cha Young Africans wanajukumu hilo, ambalo litafikiwa kwa kuwa na umoja na mshikamano katika kipindi chote cha msimu wa Ligi Kuu na michuano ya Kimataifa.
“Tuna kazi kubwa ya kufanya hiyo ni lazima iweze kukamilika, kwenye ligi tuna malengo ya kufanya vizuri kwa kupata matokeo chanya na hata kwenye mashindano ya kimataifa ni muhimu kufanya vizuri.
“Ushindani utakuwa mkubwa hilo lipo wazi lakini nasi lazima tutapambana kupata matokeo kwenye mechi zetu ambazo tutacheza, mashabiki wawe bega kwa bega nasi,” amesema Ambundo.
Young Africans itaanza mshike mshike wa Msimu mpya wa 2021/22 mwishoni mwa juma hili kwa kucheza mchezo wa hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.