Polisi nchini Uganda inamsaka James Kabariroha (62), kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi Federesi Karabaye (80), kwa madai ya kushindwa kumpa sehemu ya mali ya familia.
Kwa mujibu wa msemaji wa Polisi Mkoa wa Kigezi Elly Maate, amesema tukio hilo limetokea Juni 3, 2022 na kwamba marehemu alikuwa ni mkazi wa kijiji cha Rwentaka kilichopo Kisizi kata ya Nyarushanje wilayani Rukungiri.
“Mtuhumiwa Kabariroha ambaye ni mwalimu mstaafu wa shule ya msingi alimvamia mama yake na kumuua akipinga wosia wa marehemu baba yake aliuoacha miaka saba iliyopita ukimtenga na wale waliopaswa kupata sehemu ya mali,” amefafanua Maate.
Amesema Kabariroha pia anashukiwa kukodi watu wengine watatu ambao walimsaidia kutekeleza mauaji hayo na kwamba mwili wa marehemu ulipatikana ukiwa na majeraha kadhaa kichwani, kifuani na mgongoni.
Awali akihojiwa na Jeshi la Polisi binti wa marehemu Asiimwe Mugisha amesema walifanya kikao cha familia ambapo pamoja na mambo mengine waliazimia kuheshimu wosia wa baba yao na kwamba taarifa za kifo cha mama yake zimemshtua na kumshangaza.
“Tulifanya kikao cha familia hivi karibuni nyumbani, na kaka yangu alihudhuria na wote tukakubaliana kutobadilisha wosia lakini nilishtuka sana kusikia taarifa za kusikitisha kwamba kaka yangu alimuua mama kwa jambo ambalo tayari limetatuliwa,” amesimulia Asiimwe.
Mjomba wa mtuhumiwa Moses Guma amesema baada ya kifo cha mume wa dada yake Bi Karabaye mwanawe alikuwa akimtaka abadilishe wosia kwa sababu haukuwa ukimpendeza wala kumjali na kwamba atakosa haki yake.
Inadaiwa katika wosia aliouacha marehemu ulitaka mwanaye huyo asipewe kitu kwakua sehemu kubwa ya ardhi iliuzwa ili kumsomesha peke yake huku nduguze sita wakibaki nyumbani lakini hakurudisha fadhila baada ya mafanikio na ndipo aliazimia kumtenga kimaandishi.
“Baba yetu aliuza ardhi wakati akimsomesha na sisi wengine hatukusoma, hivyo baada ya kifo cha baba yetu, mtuhumiwa alitaka Wosia ubadilishwe ili apate ardhi lakini hiyo ilishindikana kutokana na wosia wa baba,” amehitimisha Asiimwe.
Visa vya mauaji na kujiua vimekuwa vikishamiri katika maeneo mbalimbali ukanda wa Afrika ya Mashariki ambapo hivi karibuni nchini Tanzania Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro lilisema linamshikilia mkazi wa wilaya Siha Stephano Sikawa (33), kwa tuhuma ya kumchinja hadikumuua mkewe, Sioni Daudi (26), mbele ya mwanawe (6).