Zaidi ya watu 50 wanahofiwa kufariki baada ya watu watano waliokuwa na silaha kuwafyatulia risasi waumini wa Kanisa la Mt. Francis, lililopo mji mkuu wa Jimbo la Ondo nchini Nigeria.

Akizungumza na shirika la la habari la Vanguard, mmoja wa mashuhuda amesema watu hao wasiofahamika walivamia kanisa hilo wakati wa ibada na kuwapiga risasi waumini hao siku ya Jumapili Juni 5, 2022.

“ilikuwa kama sinema walivamia kanisa na kupiga risasi kiholela wakitaka kumteka Kasisi, walirusha bomu na watu kadhaa waliuawa wakiwemo watoto na wanawake,” alisimulia shuhuda huyo.

Video za mitandao ya kijamii zilionesha maiti kadhaa nje ya Kanisa hilo na Polisi bado haijatoa taarifa rasmi ikiwemo idadi ya waliofariki katika tukio hilo la June 5, 2022.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Owo Adelegbe Timileyin, amewaambia waandishi habari kuwa Kasisi aliyekuwa anaongoza ibada ametekwa nyara na Watoto ni miongoni mwa idadi kubwa ya watu waliofariki katika shambulio hilo.

Taarifa ya Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis imetoa pole kwa wathirika na kuwaombea marehemu wote huku ikiwapa pole Wananchi.wa Nigeria kwa msiba huo uliotokea wakati wa sherehe za Pentekoste.

Tayari Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amelaani tukio hilo na kuagiza mamlaka husika kuchukua hatua na kufahamu waliohusika katika tukio hilo huku ikidaiwa majeruhi wengi wamelazwa katika Kituo cha Matibabu cha Federal kilichopo Wilayani Owo.

Hata hivyo, bado haijafahamika ni nani aliyehusika na shambulio hilo ambalo ni nadra kutokea kwenye jimbo hilo, licha ya kwamba baadhi ya majimbo ya Nigeria yamekua yakishambuliwa mara kwa mara ama na wanamgambo wenye itikadi kali au magenge ya wahuni.

Hatuuzi vidole: Serikali Zimbabwe
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Juni 6, 2022