Mkaazi wa kijiji cha Randani, Kisii nchini Kenya aliyetajwa kwa jina la James Karori mwenye umri wa miaka 22 amuawa na mdeni wake aliyekuwa anamdai kiasi cha sh 100 za Kenya, sawa na sh 2,240 za Tanzania.
Mauaji hayo yaliyowashtua wakaazi wa kijiji cha Randani yanaripotiwa kufanywa Jumamosi iliyopita na Donald Onyango aliyekuwa anamdai marehemu waliyekuwa wanafanya kazi ya ujenzi pamoja.
Mkuu wa polisi wa eneo la Kenyenya, OCPD Isaac Thuranira amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanaendelea kumsaka mtuhumiwa aliyetoroka baada ya kufanya mauaji hayo.
“Tunamtafuta mtuhumiwa aliyefanya kosa hilo kubwa la jinai. Tunawaomba raia wema wanaoweza kufahamu alipo walitaarifu jeshi la polisi.” alisema Thuranira.
Kiongozi huyo wa jeshi la polisi alisema kuwa awali mtuhumiwa huyo alikuwa amemkopesha Karori Ksh 1,000, lakini Karori alirejesha sh800. Baadaye, marehemu alimuongeza sh100, lakini alikasirishwa na kutomalizika kwa deni hilo kwa wakati huku sh 100 ikibaki.
Ameeleza kuwa Onyango alitishia kumuua Karori kwa kutomalizia deni lake, lakini baadhi ya wanakijiji walijitolea kumalizia deni hilo kuepusha shari.
Hata hivyo, wanakijiji hao walishangazwa na uamuzi wa ghafla wa Onyango aliyemfeka shingo Karori na kusababisha kifo chake palepale, kisha kutokomea kusikojulikana.