Wakati vita kati ya Real Madrid na Shirikisho la Soka la Brazil (CBF) ya kuwania huduma ya Carlo Ancelotti ikiendelea kupamba moto, Kocha huyo kutoka nchini Italia amekataa kuhusishwa kwa jambo lolote.
“Nitakupa nafasi ya kuuliza swali lingine,” Ancelotti alimwambiamwandishi wa habari katika mkutano wake na wanahabari kabla ya mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya SSC Napoli, alipoulizwa kama atakuwa katika klabu hiyo kwa msimu mwingine.
“Ninasema tena, sizungumzii juu ya maisha yangu ya baadaye.”
Huku mkataba wake na ukitarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, Rais wa CBF, Ednaldo Rodrigues, akitoa kelele za kujiamini kuhusu kumnasa Mtaliano huyo mwenye umri wa miaka 64, Real Madrid wanahaha kumsainisha mkataba mpya.
Ofisa mmoja wa klabu hiyo alithibitisha kwa Reuters, Rais wa Madrid, Florentino Pérez, anafikiria kumuongezea mkataba, huku Mkurugenzi wa CBF aliiambia Reuters wanatarajia kuwa naye kwa ajili ya mashindano ya Copa América mwaka ujao huko Marekani.
CBF inatarajia kumnasa rasmi Ancelotti ifikapo katikati ya Januari 2024, na kubatilisha kipengele cha kumalizia mkataba wake na Real Madrid kwa mwaka mwingine na kusema wana “ulinzi wa kisheria” kulinda maslahi yao endapo dili hilo litasambaratika.