Kocha Mkuu wa Real Madrid Carlo Ancelotti amelaumu udhaifu wa safu yake ya ulinzi wakati kikosi chake kilipopokea kisago cha mabao 3-1 kwenye mchezo wa dabi dhidi ya Atletico Madrid katika Ligi Kuu Hispania, La Liga, juzi Jumapili (Septemba 24).
Pamoja na kulaumu safu yake ya ulinzi, lakini alikataa kukosoa mchezaji mmoja mmoja, akisema kupoteza mchezo huo ni kosa lake kama Kocha Mkuu wa klabu hiyo kubwa barani Ulaya.
Alvaro Morata aliiweka Atletico mbele baada ya dakika nne pekee kwenye Uwanja wa Metropolitano, kabla ya Antoine Griezmann kufanya matokeo kuwa 2-0.
Toni Kroos aliifungia Real Madrid bao, lakini bao la kichwa la Morata baada ya mapumziko liliwahakikishia Atletico pointi tatu.
Matokeo hayo yanawaacha Real Madrid wakiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo na pointi zao 15, moja nyuma ya FC Barcelona na Girona huku Atletico wakiwa na pointi 10 na mchezo mmoja mkononi.
“Tatizo lilikuwa udhaifu wa ulinzi,” alisema Ancelotti katika mkutano wake na waandishi wa habari baada ya mechi. “Katika mechi sita msimu huu tulikuwa tumefungwa mabao matatu, na juzi tumeruhusu matatu ndani ya dakika 45.
“Tulikuwa tete, haukuwa usiku mzuri kwenye safu ya ulinzi. Sitamlaumu mtu mmoja mmoja, lakini hatukulinda vizuri. Hatukuwa na nafasi nzuri.
Huku Vinicius Junior akikosekana kwenye kikosi cha Real Madrid kutokana na kuchelewa kupona majeraha, Ancelotti aliamua kumchezesha Jude Bellingham kama Mshambuliaji pamoja na Rodrygo huku Luka Modric na Toni Kroos wote wakianza katika safu ya kati kwa mara ya kwanza msimu huu.
“Mfumo haukubadilika,” alisema Ancelotti.
“Tulianza na Modric kama namba 10 na washambuliaji wawili, Bellingham na Rodrygo. Labda ningefanya vizuri zaidi, wakati timu haifanyi kile ambacho ingeweza kufanya, ni wazi kwamba hilo ni jukumu langu.
Kocha wa Atletico, Diego Simeone, alisifu kiwango cha timu yake na Morata, ambaye sasa amefunga mabao matano kwenye La Liga.
“Alvaro alicheza mchezo wa kuvutia,” alisema Simeone.
“Tunamhitaji Morata huyu. Tunajua anaweza kufanya hivyo. Tunajua ana zana za kupata. Tutegemee anaweza kudumisha kiwango hiki, kwa sababu kwa Hispania na Atletico Madrid ni Mshambuliaji muhimu.
“Nina furaha sana kwa mashabiki, Morata alisema. Hali ya hamasa ilikuwa ya ajabu. Sote tulikuwa pamoja, sisi Lwanjani na wao kwenye majukwaa.”