Meneja kutoka nchini Argentina Mauricio Pochettino amebainisha maeneo matatu ambayo atahitaji kuyaimarisha endapo atakabidhiwa jukumu la kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi la Chelsea, imeelezwa.
Pochettino yupo kwenye hatua za mwisho za kuafikiana na Chelsea kwenda kuinoa timu hiyo kuanzia msimu ujao, akitarajia kuchukua mikoba ya Frank Lampard mwishoni mwa msimu.
Chelsea imekuwa na msimu wa hovyo, ikishika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England licha ya kutumia Pauni 600 milioni kwenye usajili wa madirisha mawili yaliyopita.
Ripoti zinadai Pochettino atahitaji kipa mpya, kiungo mpya na mshambuliaji mpya kwa ajili ya msimu ujao.
Hata hivyo, shida inayomkabili Pochettino, 51, timu hiyo ni lazima iondoe wachezaji kibao kabla ya kuongeza wengine kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi huko Ulaya.
Makipa wa sasa wa Chelsea ni Kepa Arrizabalaga na Edouard Mendy, lakini Pochettino anamtaka Andre Onana kutoka Inter Milan, huku akimsaka kiungo mpya pia aje kucheza na Enzo Fernandez kutokana na N’Golo Kante kuumiaumia na Mateo Kovacic anahusishwa na mpango wa kwenda Manchester City.
Pochettino, ambaye alikuwa na straika Harry Kane alipokuwa Tottenham, anahitaji Namba 9 mpya atakapotua Stamford Bridge.
Pierre-Emerick Aubameyang anahusishwa na mpango wa kurudi Barcelona, huku Romelu Lukaku akitarajia kurudi kutoka kwa mkopo Inter, lakini Pochettino anataka straika mwingine na Victor Osimhen akiwekwa kwenye mipango. Lakini, Chelsea itamkaribisha pia Christopher Nkunku kwenye kikosi chao akitokea RB Leipzig.