Kiungo na nahodha wa mabingwa watetezi wa ligi ya soka nchini Hispania FC Barcelona Andres Iniesta, huenda akatimka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32, bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu ambao unamuwezesha kuendelea kuitumikia FC Barcelona, lakini endapo klabu yoyote itaonyesha dhamira ya kuvunja mkataba huo, huenda akaondoka na kwenda kusaka changamoto mpya ya soka lake.

Jarida la michezo la Don Balon, limeitaja klabu ya New York City FC inayoshiriki ligi ya nchini Marekani (MLS), kuwa katika harakati za kuwasilisha ofa ya kumsajili kiungo huyo, ambaye tayari ameshaitumikia Barca katika michezo 403 na kufunga mabao 34.

Klabu ya New York City ambayo ina ushirika na Manchester City ya England kufuatia mmiliki wake kuwa mmoja, imeanzisha mchakato wa kutaka kumsajili Iniesta kwa kutumia uzoefu wa  mkurugenzi wake wa ufundi Ferran Soriano, ambaye aliwahi kufanya kazi Camp Nou yalipo makao makuu ya FC Barcelona.

Uongozi wa New York City unadaiwa kutumia mbinu za ukaribu uliopo kati ya Iniesta na David Villa ili kufanikisha mpango wa usajili huo mwishoni mwa msimu huu.

Mwezi uliopita Iniesta alikataa kuelekea China, ambapo moja ya klabu za soka nchini humo, ziliripotiwa kumtengea kiasi cha pauni milioni 34 kama ada yake ya usajili.

Video: Rais Magufuli Amtaka Makonda Aendelee Kuchapa Kazi
Video: Waziri Nape asema hana faida kama uhuru wa habari unaingiliwa, aunda kamati