Mshambualiji Ihefu FC Andrew Simchimba ameoteshwa ufungaji bora, licha ya timu yake kuondoshwa kwenye kombe la shirikisho ‘ASFC’ hatua ya Robo Fainali.
Pamoja na kutolewa na Simba SC kwa mabao 5-1, timu hiyo ya wilayani Mbarali, lakini staa wake Simchimba ndiye kinara wa mabao akiwa amefunga mabao saba akimuacha mpinzani wake Clement Mzize wa Young Africans mwenye mabao sita.
Simchimba amesema licha ya malengo yao ya timu kutofikia lakini anaamini anaweza kuibuka mfungaji bora kutokana na hatua iliyofikia kwa sasa timu zote ni kama zinalingana uwezo hivyo vita itakuwa ngumu.
Amesema kuwa alihitaji kufunga zaidi ya mabao saba na kufikisha walau kumi lakini anashukuru kwa kile alichokipata na kwamba nguvu sasa anazielekeza kwenye ligi kuu kuongeza idadi.
“Nilihitaji kuzidi hapo ila kuondolewa kwetu nadhani haiwezekani tena, ila naamini naweza kuwa mfungaji bora, timu zilizofuzu ni kama nguvu sawa, hakuna ile kufungana mabao mengi,” amesema Simchimba.
Nyota huyo ameongeza kuwa siri ya mafanikio kikosini ni ushirikiano wa ndani na nje ya uwanja na kwamba kuuanzá msimu vibaya ni matokeo ya mpira lakini hawakuwa vibaya.
“Matokeo ya sasa yanatupa hamasa kubwa, lakini kikubwa ni kujituma kwa kila mmoja na kushirikiana wote, tunaendelea kupambana kuhakikisha tunamaliza nafasi nzuri,” amesema mshambuliaji huyo