Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limefuta matokeo ya kidato cha nne ya shule ya sekondari ya seminari ya Malinyi ya Mkoani Morogoro baada ya kubaini kuwa ilifanya udanganyifu.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dkt. Charles Msonde ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma akitangaza matokeo hayo.
Dkt. Msonde ameeleza kuwa shule hiyo ilibainika kuvujisha kwa makusudi mitihani hiyo, hivyo wanafunzi 57 waliofanya mitihani katika kituo hicho wamefutiwa matokeo.
Amesema kuwa Baraza hilo limeagiza kuwasakwa wote waliohusika na udanganyifu huo ikiwa ni pamoja na askari wa jeshi la polisi waliokuwa wanalinda katika kituo hicho ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Kituo cha mitihani kilichokuwa kwenye shule hiyo pia kimefutwa kama sehemu ya adhabu ya awali, kwa mujibu wa Dkt. Msonde.
Matokeo yaliyotangazwa leo yameonesha kupanda kwa wastani wa ufaulu kwa asilimia 1.29 ukiwa ni asilimia 78.38 kutoka 77.09 ya mwaka uliopita.