Chama kikuu zaidi cha upinzani nchini Angola UNITA, kimesema kitapinga matokeo ya uchaguzi wa Urais wa nchi hiyo ambao ulimalizika kwa chama tawala cha muda mrefu cha MPLA kukishinda kwa wingi wa kura.
Uchaguzi huo, uliofanyika Agosti 24, 2022 na matokeo yaliyotangazwahapo jana Agosti 29, 2022 na kuiweka Movement for the Liberation of Angola (MPLA), kama mshindi kwa kupata asilimia 51.17 ya kura, hivyo kumpata Rais Joao Lourenco muhula wa pili.
Katibu Mkuu wa National Union for the Total Independence of Angola (UNITA), Alvaro Chikwamanga Daniel amesema hawatambui matokeo ya tume ya taifa ya uchaguzi na watawasilisha madai ya kisheria yatakayosimamisha tangazo la matokeo ya mwisho.
Wakati wa awamu ya mwisho ya zoezi la kuhesabu kura, chama hicho kinadai hakikujulishwa uamuzi na tume ya uchaguzi ili kuridhia matokeo na kwamba hakikupokea nakala ya majedwali ya matokeo ya mwisho.
Wagombea wa uchaguzi huo, wana saa 72 baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kuwasilisha madai kwa mahakama ya kikatiba kupinga kura hiyo huku Makamishna wanne kati ya 16 wa uchaguzi wakiwa hawajasaini matokeo ya mwisho, kwa madai ya kuwa na mashaka kuhusu mchakato huo.
MPLA, kimekuwa chama pekee kinachotawala nchi hiyo tangu ilipojinyakulia uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1975, lakini kimekuwa na matokeo mabaya zaidi ya kura za mwaka huu, chini ya ushindi wake wa asilimia 61 kwa mwaka 2017.
UNITA ilipata mafanikio makubwa kutokana na uchaguzi wa 2017, baada ya kupata asilimia 43.95 ikilinganishwa na asilimia 26.67 katika kura za awali na inadaiwa kuwa chini ya nusu ya takriban wapiga kura milioni 14.4 waliosajiliwa walishiriki upigaji kura wa vyama vinane vilivyoorodheshwa.