Mwanamke mmoja aliyeachwa peke yake ndani ya ndege baada ya kulala usingizi mzito akiwa safarini kwa kutumia shirika la ndege la Canada kutoka jiji la Quebec kwenda Toronto ameathirika na tukio hilo kwa kuanza kuota ndoto za kutisha usiku.
Tiffani Adams alisafiri juni 9 mwaka huu na alipopanda ndege alipitiwa na usingizi, alipoamka alijikuta yumo ndani ya baridi kali, huku bado akiwa amefunga mkanda wa kiti chake, lakini ndege ilikuwa imeegeshwa na taa zote zimezimwa.
Kwamujibu wa taarifa aliyoitoa Adams kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook amesema kuwa amekuwa akipatwa na ndoto za kutisha toka tukio hilo lilipomtokea.
“mishale ya saa sita usiku saa chache baada ya ndege hiyo kutua, nilikuwa kwenye baridi kali huku nikiwa bado nimechomeka mkanda wangu kitini, na kiza totoro” aliandika Adams.
Nakuongeza kuwa halihiyo ilikuwa ya kuogopesha, huku shirika la ndege la Canada likiwa limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanafanya uchunguzi.
Mama huyo alifanikiwa kumpigia simu rafiki yake, Deanna Dale na kumfahamisha mahali alipo na kwa bahati mbaya simu yake ilizimika kwa kuishiwa chaji na hakuweza kuchaji simu yake kwani ndege ilikuwa imezimwa.
Rafiki wa mwanamke huyo, Dale alifanikiwa kuwapigia simu polisi wa uwanja wa ndege wa Toronto Pearson na kuwaarifu juu ya masaibu ya rafiki yake mahali alipokwama.
Kwa bahati nzuri Adams akiwa bado amekwama kwenye ndege aliweza kuona kurunzi (tochi) kwenye eneo la rubani na akajaribu kuiwasha ili watu waone kuna kitu ndani ya ndege hiyo.
Baada ya muda aliwaona dereva wa magari madogo ya kupakua mizigo ya wasafiri, ambao walipigwa na butwaa kumuona.
Amesema kuwa wafanyakazi wa shirika la ndege la Canada walimpatia gari la kifahari na chumba cha hoteli baada ya kumnasua kutoka kwenye ndege hiyo lakini alikataa, akataka kurejea nyumbani kwa haraka.
Hadi sasa tayari mwakilishi wa shirika hilo ameshampigia simu mara mbili kwa uchunguzi na kuomba radhi kwa tukio hilo.