Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Young Africans, Arafat Haji ameibuka tena na kusisitiza hatokua tayari kuona kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajibu anasajiliwa klabuni hapo kwa msimu ujao wa Ligi Kuu na michuano ya Kimataifa.
Arafat ameshikilia msimamo wake, akidai kwa timu wanayoiandaa msimu ujao, kiungo mshambuliaji huyo hana nafasi kwa kiwango alichonacho kwa sasa.
Hata hivyo kiongozi huyo ameonesha kuheshimu mchango wa Ajib alipokua Young Africans, kwa kusema alifanya mambo makubwa kwa kuisaidia klabu hiyo, lakini msimu ujao haini nafasi yake kwenye kikosi cha klabu hiyo.
“Amecheza misimu miwili aliisaidia timu kwa namna moja au nyingine sasa sio muda wake tena, kiwango cha kuitumikia timu yetu inayoandaliwa kwa ajili ya ushindani hana na nilipambana kuzungumzia suala la kiungo huyo mitandaoni nikiwa kama mmoja wa viongozi wa klabu na sio mdau,” amesema na kuongeza kuwa:
“Wanayanga walikoseshwa amani na madalali ambao walikuwa wanatumia vibaya nafasi zao kuweza kudanganya ili ajenda zao zifanikiwe na ndipo nilipotoka na kuwaondoa hafu,”
“Mara nyingi watu wanaofanya hivyo sio wale wanaoipenda timu, wapo kuitumia ili iwanufaishe wao binafsi, nawapa rai wanayanga wawakatae watu wa namna hii ili kuifikisha timu yetu mbali na iwe ni miongoni mwa timu bora barani Afrika.”
Mkataba wa Ajib na Simba SC tayari umeshafikia kikomo, huku tetesi zikieleza kuwa kiungo huyo huenda asisaini mkataba mpya kwa mabingwa hao wa Tanzania Bara mara nne mfululizo.