Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi, amesema wanakwenda nchini Urusi wakiwa na matumaini makubwa ya kufanya vyema, kufuatia kuwa na mwenendo mzuri wa maandalizi wanayoyafanya hivi sasa.
Messi ametoa kauli hiyo baada ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa leo alfajiri kwa saa za Afrika mashariki dhidi ya Haiti kwenye uwanja wa Boca Junior mjini Buenos Aires, ambao umeshuhudia wakishinda mabao manne kwa sifuri.
Katika mchezo huo Messi amefunga mabao matatu pekee yake (Hat-Trick), huku bao moja akimtengenezea mshambuliaji mwenzake Sergio Aguero.
“Hatuendi kwenye fainali za kombe la dunia kama taifa linalopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa, tunakwenda na matumaini ya kushindana na yoyote tutakaekutana naye,” Amesema Messi.
“Mchezo wetu dhidi ya Haiti umeonyesha namna maandalizi tuliyoanza kuyafanya kwa fainali za 2018 yalivyo mazuri, pia mchezo huu umekua sehemu ya kuwaaga mashabiki wetu ambao hawatoambatana nasi kuelekea nchini Urusi,” ameongeza Messi. “Tuna kikosi kamili kilichokua tayari kupambana na yoyote na wakati wowote.”
Kikosi cha Argentina kinatarajia kuasafiri kuelekea mjini Barcelona, Hispania kuendelea na kambi ya maandalizi ya fainali za kombe la dunia, na baadae kitasafiri hadi nchini Urusi kwa ajili ya mapambano ya kundi D, ambapo kitaanza mshike mshike huo kwa kucheza dhidi ya Iceland Juni 16, kisha Croatia Juni 21 na kitamaliza michezo ya hatua ya makundi kwa kupambana na Nigeria Juni 26.