Baraza la Seneti la Argentina, limepitisha muswada wa sheria wa kihistoria unaohalalisha utoaji wa mimba kwa hiari katika Taifa hilo ambalo Kanisa Katoliki limekuwa na ushawishi mkubwa kwa muda mrefu.
Muswada huo ulipendekezwa na Rais Alberto Fernandez na ulipitishwa katika Mabaraza ya chini Desemba 11, licha ya upinzani mkali kutoka katika Kanisa Katoliki na makanisa ya Kievanjelisti yanayodai hatua hiyo ni kinyume na mafundisho ya Dini.
Muswada huo unawaruhusu wanawake kutoa mimba, hadi muda usiopita wiki 14 tangu kupata ujauzito.
Serikali ya Argentina inasema kati ya matukio 370,000 na 520,000 ya utoaji mimba kinyume na sheria hurekodiwa nchini humo kila mwaka, katika taifa hilo lenye watu milioni 44.
Miaka miwili iliyopita, muswada kama huo ulipitishwa katika Mabunge ya chini, lakini ukaangushwa baadaye katika Baraza la Seneti na sasa Argentina imekuwa miongoni mwa kundi dogo la nchi za Amerika Kusini kuchukua hatua hiyo.