Armenia na Azerbaijan leo zimelaumiana kwa kukiuka mkataba wa kusitisha mapigano kwenye jimbo lenye mzozo la Nagorno Karabakh muda mfupi tangu makubaliano hayo yalipoanza kufanya kazi asubuhi ya leo.
Wizara ya Ulinzi ya Azerbaijan imesema kuwa wanajeshi wake katika kijiji cha Safiyan walifyetuliwa risasi madai ambayo hata hivyo yamekanushwa na viongozi wa vuguvugu la kutaka kujitenga katika jimbo la Karabakh.
Kwa upande wake wizara ya ulinzi ya Armenia imeituhumu serikali mjini Baku kwa kufanya upotoshaji huku ikadai vikosi vya Azerbaijan vilifyetua makombora dakika 45 tangu kuanza kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Mkataba wa kusitisha vita ambao ni wa tatu tangu kuanza kwa makabiliano ya kijeshi kati ya Armenia na Azerbaijan, uliafikiwa mjini Moscow chini ya uratibu wa Marekani na pande zote mbili ziliahidi kuheshimu utekelezaji wake.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesisitiza ombi lake kwa Armenia na Azerbaijan la kusitisha mapigano hayo pia ameziomba pande zote mbili kuruhusu uingizwaji wa misaada ya kibinadamu.
Kwa mujibu wa maafisa wa mkoa huo, wanajeshi wao 974 na raia 37 wameuawa katika makabiliano hayo mpaka sasa.