Armenia imeanza maombolezo ya siku tatu leo Desemba 19, kuwaenzi wahanga wa mapigano na Azerbaijan huku upinzani ukizidisha shinikizo la kumtaka kiongozi wa nchi hiyo kujiuzulu kwa jinsi alivyoshughulikia mzozo huo.
Katika siku hii ya kwanza ya maombolezo, Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan ameongoza maandamano hadi uwanja wa kumbukumbu kwenye mji mkuu, Yerevan, ambako wahanga wa mapigano hayo walizikwa.
Upande wa upinzani ulipanga kufanya maandamano tofauti leo Desemba 19, 2020 huku wakitoa wito wa kufanyika mgomo wa taifa zima kuanzia Desemba 22.
Zaidi ya watu 5,000 waliuawa nchini Armenia na Azerbaijan wakati mapigano yalipozuka kati ya mahasimu hao wakiwania udhibiti wa jimbo la Nagorno Karabakh.
Mzozo huo ulimalizika mnamo mwezi Novemba baada ya kufikiwa makubaliano mjini Moscow, yaliyowezesha Armenia kuliachia jimbo la Nagorno Karabakh kwa Azerbaijan.