Meneja mpya wa klabu ya Arsenal Unai Emery huenda akafanya usajili mwingine kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi ya England mnamo August 10.
Meneja huyo anahusishwa na taarifa za kutaka kumsajili mshambuliaji kutoka nchini Senegal M’Baye Niang, baada ya klabu yake ya Torino kufuta mpango wa kumsainisha mkataba mpya.
Wakati mpango huo ukifutwa, tayari Niang ameshazitumikia baadhi ya klabu barani Ulaya kwa mkopo, kutokana na kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza akiwa na klabu ya AC Milan tangu mwaka 2012.
Klabu alizozitumikia kwa mkopo ni Montpellier (2014) alicheza michezo 19 na kufunga mabao 4, Genoa (2015) michezo 14 mabao 5, Watford (2017) michezo 16 mabao 2, Torino (2017 –2018) michezo 26 mabao 4.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23, aliyekua kivutio wakati wa fainali za kombe la dunia, aliwahi kuhusishwa na taarifa za kutakiwa na klabu ya Arsenal misimu kadhaa iliyopita wakati wa utawala wa meneja Arsene Wenger, lakini hakufanikiwa kutua Emirates Stadium.
Hata hivyo klabu ya Nice ya Ufaransa nayo imeonyesha nia ya kumsajili kwa mkopo, lakini upande wa Arsenal upo tayari kumsajili jumla, kwa ada ya Pauni milioni 12.5.