Vinara wa Ligi Kuu ya England Klabu ya Arsenal imefanya mazungumzo na Shakhtar Donetsk yaUkraine ili kufanikisha usajili wa Kiungo Mshambuliaji Mykhaylo Mudryk.
Taarifa zilizotolewa na Tovuti ya 90min imeeleza kuwa, Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21, ni mmoja wa washambuliaji wanaohitajika sana Ulaya hivi sasa, na Shakhtar wako tayari kumuuza, lakini kwa bei sahihi tu.
Shakhtar wamesema hadharani kwamba Mudryk kwa sasa thamani yake ni euro milioni 100.
“Yeyote anayetaka kumsajili Mudryk lazima alipe kiasi kikubwa cha fedha, vinginevyo hatuwezi kumuuza,” amesema Mkurugenzi wa Soka wa Donetsk, Darijo Srna mwishoni mwa wiki.
Mudryk mwenyewe hajaficha nia yake ya kutaka kuhama na alikuwa karibu kujiunga na Brentford katika majira ya joto na kisha akaona dili linalowezekana na Bayer Leverkusen likishindikana.
Klabu ya AC Milan, Juventus, Ajax na Newcastle United pia zimemtazama kwa karibu katika miezi ya hivi karibuni, lakini 90min inaelewa kuwa Arsenal sasa wanaonekana kuongoza katika mbio za kumnasa.
‘Washikabunduki’ hao wamelenga kusajili fowadi mpya wakati wa dirisha la Januari baada ya kushindwa kumpata Raphinha majira ya joto.
Pia, wanamtaka kiungo na beki, lakini mshambuliaji mpya anaibuka kama kipaumbele chao cha kwanza.
Moussa Diaby, Christian Pulisic na Joao Felix pia wamejadiliwa na uongozi wa klabu hiyo, lakini Mudryk ndiye mchezaji ambaye anaonekana kuhitajika zaidi.
Vyanzo vya karibu na Arsenal vinaamini kuwa wako tayari kuvunja rekodi ya klabu yao ili kumleta Mudryk Kaskazini mwa London, lakini inabakia kuonekana kama wanaweza kukubaliana na Shakhtar.