Meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger ameendelea kusisitiza hatomuuza mshambuliaji wake kutoka nchini Chile Alexis Sanchez katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi.

Wenger amesisitiza suala hilo, kufuatia kauli iliyotolewa na mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa yupo kwenye mapumziko baada ya kuitumikia timu yake ya taifa kwenye michuano ya kombe la mabara, ya kutaka kucheza ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao.

Arsenal haitoshiriki michuano hiyo, baada ya kumaliza katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ya England msimu uliopita, hivyo itacheza michuano ya Europa League.

Sanchez mwenye umri wa miaka 28 amesaliwa na mkataba wa mwaka mmoja wa kuitumika Arsenal, na mpaka sasa mustakabali wa kusainishwa mkataba mpya klabu hapo bado ni kizungumkuti.

“Msimamo nilioutangaza siku za nyuma kuhusu Sanchez sitoubadilisha,” Wenger aliwaambia waandishi wa habari nchini China ambapo kwa sasa kikosi chake kimeweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi ya England.

“Kuhusu ushiriki wetu kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, tumeshiriki huko kwa miaka 20, miaka 17 ilikua kabla ya kusajiliwa kwa Sanchez, naimani kwa maelezo haya nitakua nimeeleweka.”

“Siwezi kuendelea kuzungumza suala hili kila kukicha, wakati msimamo wangu na wa klabu umeshaelezwa wazi, hivyo ninashauri jambo hili lifungwe rasmi,” Aliongeza Wenger.

“Mtazamo wetu kwa sasa ni kujiandaa vyema na msimu mpya wa ligi, na tumeanza kufanya hivyo tangu juma lililopita, ninaamini katika hili tutafanikiwa.”

Katika hatua nyingine Wenger akalazimika kujibu swali ambalo aliulizwa na waandishi wa habari kuhusu kauli ambazo huzitoa pale mchezaji wake anapokua mbioni kuondoka, akipewa mfano wa aliyekua mshambuliaji wake kutoka nchini Uholanzi Robin van Persie aliyetimkia Manchester United mwaka 2012 baada ya kugoma kusaini mkataba mpya.

“Suala la Van Parsie lilikua tofauti na hili la Sanchez, Van Persie alilazimika kuondoka na tukakubaliana naye, kutokana na umri wa miaka 30 aliokua nao kwa kipindi hicho, tuliamini asingeweza kutusaidia kwa kipindi kirefu,”

“Sanchez bado ni kijana mdogo, ana umri wa miaka 28.” Amesema Wenger.

 

Kikosi cha Arsenal leo kitacheza mchezo wake wa kwanza tangu kilipotua nchini China dhidi ya mabingwa wa soka nchini Ujerumani Bayern Munich .

Kisa cha mke kufyeka sehemu za siri za mumewe
Mghwira amvaa Lowassa, asema kuhama chama ni ufisadi wa kisiasa