Meneja wa klabu ya Arsenal Arsène Wenger amesema ataendelea kufanya usajili katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi, baada ya kukamilisha uhamisho wa mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Alexandre Lacazette.
Wenger yupo katika mawindo ya kumsaka mshambuliaji wa pembeni wa mambingwa wa soka nchini Ufaransa AS Monaco Thomas Lemar, ambaye thamani yake inakadiriwa kufikia Pauni milioni 40.
Tayari ofa ya Arsenal ya Pauni milioni 30 iliyomlenga mchezaji huyo imeshakataliwa na viongozi wa AS Monaco, kwa madai haina thamani sahihi na uwezo wa Lemar, ambaye alikua chachu ya kupatikana kwa ubingwa wa Ufaransa msimu uliopita.
Wenger ameiambia tovuti ya Arsenal kuwa “Bado tupo katika mpango wa kuendelea kufanya usajili katika kipindi hiki, na huenda asiwe mchezaji mmoja ama wawili.
“Siwezi kusema ni wapi tunapoelekea kwa sasa, lakini ninawahakikishia mashabiki wa Arsenal kuwa, tutasajili wachezaji wenye hadhi kubwa ambao wana uwezo wa kucheza soka la ushindani kwa msimu mzima.
Kauli hiyo ya Wenger imeshtukiwa na vyombo vingi vya habari, kwa kuhisi alikua anazungumzia uwezekano wa kumsajili Lemar ambaye ameonyesha kuwa na shauku ya kumsajili.
Juma lililopita mzee huyo wa kifaransa alivunja rekodi ya usajili ndani ya klabu ya Arsenal, kwa kumsajili mshambuliaji Alexandre Lacazette kwa dau la Pauni milioni 52 akitokea Olympique Lyonnais.