Kocha Mkuu wa Singida Fountain Gate, Hans Pluijm amesema amefurahishwa na kiwango kilichooneshwa na timu hiyo kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambapo waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Timu hiyo ilitumia mchezo huo kutambulisha nyota wake kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na michuano ya kimataifa ambapo timu hiyo itashiriki Kombe la Shirikisho la Soka Barani Afrika.
Pluijm amesema wachezaji wake walionesha kiwango cha kuvutia, hali inayompa matumaini ya kufanya vizuri kwenye mashindano yote msimu ujao.
“Walicheza vizuri, walijitoa na nidhamu ya hali ya juu ya mchezo. Kile ambacho wamekionesha wakiendelea nacho tutafanya vizuri mashindano yote tutakayoshiriki,” amesema kocha huyo wa zamani wa Young Africans.
Singida Fountain Gate ilitambulisha wachezaji 29 itakaowatumia kwenye Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu ujao.
Tayari Singida Fountain Gate imeanza safari ya kuelekea jijini Tanga kwa ajili ya Ngao ya Jamii ambako watacheza Alhamisi ijayo dhidi ya Simba SC.