Mabingwa wa soka Tanzania bara Young Africans watalazimika kusafiri kwa mara ya tatu mfululizo kwenda kucheza ugenini katika michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC), safari hii wakiwafuata Singida United katika Robo Fainali Uwanja wa Namfua mjini Singida.
Hiyo ni baada ya droo ya michuano hiyo iliyioangwa mapema hii leo katika studio za Azam TV, Tabata mjini Dar es Salaam kuanzia hatua ya Robo Fainali hadi Fainali.
Droo iliendeshwa na wachezaji wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, wote mabeki George Masatu aliyewika Simba SC na Yahya Issa aliyewahi kuchezea Young Africans, chini ya usimamizi wa Ofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jemedari Said.
Baada ya kuitoa Reha FC ya Temeke Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam katika mechi ya hatua ya timu 64 ambayo pia walikuwa wageni, Young Africans ilisafiri kwenda Mbeya kucheza na Ihefu katika hatua ya 32 Bora, ikasafiri kwenda Songea kucheza na Maji Maji katika hatua ya 16 Bora na sasa itasafiri tena kwenda Singida katika hatua ya Nane Bora.
Mechi nyingine za Robo Fainali zitakuwa kati ya Azam FC watakaokuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar, Stand United watakaoikaribisha Njombe Mji FC na Tanzania Prisons watakaokuwa wenyeji wa JKT Tanzania.
Mechi za Robo Fainali zitachezwa kati ya Machi 30 na Aprili 1, mwaka huu katika viwanja vya Namfua, Singida, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Sokoine mjini Mbeya na CCM Kambarage, Shinyanga.
Mshindi kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar atakutana na mshindi kati ya Stand United na Njombe Mji FC na mshindi kati ya Singida United na Young Africans atakutana na mshindi kati ya Tanzania Prisons na JKT Tanzania katika Nusu Fainali zitakazochezwa kati ya Machi 16 na 18.
Fainali itakuwa kati ya Azam, Mtibwa, Stand na Njombe ambayo timu itakayofuzu hatua hiyo itakuwa mgeni wa Singida, ama Young Africans, Prisons au JKT katika mechi ya kuhitimisha msimu wa mashindano ya ASFC kati ya Mei 30 na 31, mwaka huu.
Bingwa wa mashindano haya, Simba SC alitolewa katika hatua ya timu 64 na Green Warriors ya Mwenge iliyokuwa Ligi Daraja la Pili – na hatua ya 16 Bora ikaondoka na mshindi wa pili, Mbao FC.
Young Africans na Azam FC ndizo timu pekee zilizobaki mashindanoni ambazo zilicheza Nusu Fainali msimiu uliopita zikitolewa na Simba na Mbao.
Droo ya leo ilihudhuriwa na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Ahmed Iddi ‘Msafiri Mgoyi’ na Lameck Nyambaya pamoja na wawakilishi wote wa klabu nane zilizotinga Robo Fainali.