Jeshi la Polisi Mkoa Arusha linamshikilia Dickson Mungulu, aliyetuma ujumbe mfupi wa maneno (SMS) wa taarifa za uongo kwa ndugu zake kwamba ametekwa na waliomteka wanahitaji milioni 3 wamuachie huru la sivyo watamuuwa, kumbe fedha hizo alikuwa akizihitaji ili alipe madeni.
Taarifa hiyo imetolewa jana Julai 29, 2021, na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Justine Masejo, ambapo amesema kuwa taarifa ya kijana huyo kutekwa ilitolewa Julai 25 kutoka kwa mmoja wa ndugu ambaye jina lake limehifadhiwa akieleza kuwa ndugu yao Dickson Mungulu, ametekwa.
Mara baada ya taarifa hiyo jeshi la polisi lilifanya uchunguzi na kisha kumkamata kijana huyo aliyesadikika kupotea na baada ya mahojiano walibaini kwamba mwaka 2020 alimaliza Shahada ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Makumira kilichopo Arusha.
Sambamba na hilo baada ya kumchunguza zaidi katika mwili wake ilibainika kuwepo na majeraha sehemu ya shingo na mguu alikiri kujichoma na kitu chenye ncha kali yeye mwenyewe kwa nia ya kuwaaminisha wazazi wake pamoja na ndugu zake wengine kwamba alitekwa.