Mahakama nchini Misri imewahukumu kifungo cha kati ya miaka mitatu na mitano jela, askari 13 walioshiriki maandamano ya kudai nyongeza ya mishahara na mazingira bora ya kazi.
Askari 11 kati ya hao walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na wawili walihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kufanya uchochezi wakati wa maandamano yao ya mwaka 2015.
Mahakama ya Makosa ya Jinai iliyoko jijini Cairo, Jumamosi hii ilitoa pia nakala ya hukumu ya askari hao, iliyoripotiwa na mtandao maarufu wa Al-Ahram. Watu hao wanayo nafasi ya kukata rufaa.
Mwaka 2015, mamia ya askari wa jeshi la polisi walifanya mgomo na kushiriki maandamano wakipinga mishahara midogo na mazingira ya kazi yasiyo bora, kusini kaskazini mwa jimbo la Sharqiya.
Misri ilipitisha sheria inayopiga marufuku maandamano yoyote yasiyokuwa na kibali, mwaka 2013 baada ya jeshi kupindua utawala wa rais aliyechaguliwa.