Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni amewapandisha vyeo maofisa wawili wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha wanaofanya kazi katika kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia baada ya kutoa huduma bora kwa watalii.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kituo hicho cha Polisi, jijini Arusha, leo Juni 17, Waziri Masauni amewataja aliowapandisha vyeo kuwa ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Waziri Tenga ambaye amepandishwa kuwa Mrakibu wa Polisi (SP) na Mkaguzi wa Polisi INSP Anthony Mwaihoba ambaye amepandishwa kuwa Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP).

 “Leo asubuhi nimepokea barua toka ubalozi wa Tanzania Nchini Italia ambayo iliandikwa na watalii raia wa Italia waliofika nchini hivi karibuni kwa ajili ya shughuli za utalii,” alieleza Waziri Masauni.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na baadhi ya Askari wa Kituo cha Polisi Utalii na Diplomasia, wakati alipotembelea kituo hicho jijini Arusha, kwa ajili ya kuwapongeza Maofisa wawili waliofanya vizuri kwa kutoa huduma bora kwa Watalii.

Amefafanua kuwa, katika barua hiyo watalii hao wametoa shukrani na pongezi baada ya kuridhishwa na huduma bora waliyoipata kutokana na changamoto za kiusalama walizokua nazo ikiwemo utapeli ambapo maofisa hao walifanya juhudi kubwa za kudhibiti uhalifu huo.

“Askari hao wamekua mfano bora wa kuigwa kwa kuitangaza Nchi yetu vizuri Kimataifa hususani kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anautangaza utalii kupitia filamu ya The Royal Tour.” Alisisitiza Masauni.

Aidha amesema Serikali itandelea kuwathamini na kuwapongeza Askari wote wazalendo na waadilifu wanaotekeleza majukumu yao vizuri popote Nchini.

Sambamba na hilo ametoa wito kwa Askari wengine kufanya kazi kwa uadilifu, uzalendo na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele. Pia amekemea vitendo viovu kwa baadhi ya Askari wachache ambao sio waadilifu, ambapo amewataka kuacha tabia hizo kwani zinachafua taswira ya Jeshi la Polisi na nchi kwa ujumla.

Wasiorejesha mikopo wasakwa
Habari kuu kwenye magazeti ya leo Juni 17, 2022