Wataalam wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, wametakiwa kufuatilia vikundi vya Wanawake, Vijana na wenye Ulemavu vilivyokopeshwa Shilingi Milioni 150 ambazo bado hazijarejeshwa.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga ametoa wito huo katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani lililokuwa likipitia majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha 2020/21.

“Waliokopa ni lazima mzirejeshe fedha hizo kwa sasabu Halmashauri inaonyesha Shilingi Milioni 150 zimekopeshwa katika vikundi lakini hadi sasa fedha hizo bado hazijarudishwa,” amesema Sendiga.

Aidha, amesema kuwa Serikali ililenga kusaidia vikundi hivyo kwa kuwapa mkopo ili wapate mitaji ya kufanya shughuli zao, sambamba na kutoa ajira kwa wingine.

“Wataalam wanapaswa kuhakikisha fedha hizo zinafuatiliwa kwa ukaribu katika makundi hayo ili zirerejeshwe maana hii ni mikopo na inatakiwa kukopeshwa katika makundi mengine,” amesema sendiga.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza Halmashauri ya Mafinga Mji kwa kupata hati safi kwa miaka sita mfululizo, kutoka kwa mkaguzi wa hesabu za Serikali (CAG) ambayo imeendelea kuupatia heshima mkoa wa Iringa.

Sendinga amesema, kufanya kazi kwa ushirikiano kumepelekea Halmashauri hiyo kupata hati safi na kwamba huo umekuwa ni mfano kwa halmashauri nyingine za mkoa huo.

Aidha, amewataka watumishi wa Halmashauri ya Mafinga Mji kuendelea kufanya kazi kwa kujituma na kumuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Mafinga Mji kuwachukulia hatua za kisheria watumishi ambao wamekuwa wazembe kazini.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Saad Mtambule alisema wamekuwa wakifanya vizuri kwenye ukusanyaji mapato, kutokana na ushirikiano mzuri baina ya wafanyakazi.

“Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mafinga Mji amekuwa kiunganishi kikubwa baina ya wakuu idara na wafanyakazi wengine wa Halmashauri kuwa kitu kimoja katika kufanya kazi,” amesema Mtambule.

Naye mkurugenzi wa Hhalmashauri ya Mafinga Mji, Happiness Laizer amemuambia Mkuu huyo wa Mkoa kuwa wameyapokea maagizo yote na wanaahidi kuyafanyia kazi ili kuhakikisha kzi inasonga inaendelea.

Walinda amani wa Tanzania watoa msaada wa vifaa Lebanon
Askari walioimarisha ulinzi kwa watalii wapandishwa vyeo