Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa amewaagiza Wakuu wa Shule nchini kuwashirikisha mchakato wa upangaji wa michango mbalimbali Wazazi na Walezi kabla ya utekelezaji wa zoezi hilo.

Bashungwa ameyasema hayo hii leo Juni 16, 2022 Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ulyankulu kwa Chama cha Mapinduzi (CCM), Bi. Rehema Migila.

Katika swali lake, Mbunge huyo alitaka kujua Serikali pamoja kuondoa ada kwa wanafunzi kwa elimu msingi, bado kumekuwepo na michango mingi ambayo ni kero kwa wazazi akitolea mfano mchango wa chakula na hivyo ina kauli gani juu ya suala hilo.

“Wanafunzi wanatakiwa kutoa michango na inapotokea mzazi ameshindwa kuchangia mtoto anaadhibiwa, Serikali ina kauli gani kwa shule zinazotoa adhabu kwa wanafunzi ambao wameshindwa kulipa michango yao badala ya wazazi,”amesema Rehema.

Hata hivyo, Waziri Bashungwa amesema upo mwongozo kwa kamati za Shule unaoonesha zinatakiwa kuwashirikisha wazazi na walezi katika mchakato wa kupanga michango na hivyo ni vyema kuwashirikisha.

“Ningependa kutoa maelekezo kwa Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kushirikisha Wazazi ama Walezi kupitia mwongozo ambao tumeutoa wa namna ambayo tunawashirikisha kwenye ile michango ambayo tunahitaji kuwashirikisha,” amefafanua Bashungwa.

Aidha, amewaagiza Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu wa Shule kuwashirikisha Wazazi, Bodi za Shule, Kamati za Shule na Walezi kwa kuzingatia taratibu zilizopo.

Moses Phiri aahidi makubwa Simba SC
Wahimizwa kupunguza unywaji chai kuokoa uchumi