Jeshi la Polisi nchini Uganda limewakamata na kuwaweka karantini ‘ya selo’ askari walioonekana kwenye kipande cha video iliyochukuliwa eneo la mpaka wa nchi hiyo na Kenya, wakiwaruhusu madereva wa malori kuingina nchini humo bila kupima virusi vya corona; baada ya kupewa rushwa.
Mwendesha pikipiki asiyefahamika ndiye aliyerekodi tukio la askari hao waliokuwa mpakani wakipokea mzigo ambao haukuonekana moja kwa moja, lakini waliruhusu lori hilo kupita. Askari hao wamewekwa karantini na wanatarajiwa kupimwa covid-19 kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Emmanuel Ainebyoona amesema kuwa maafisa hao wawili pia hawakuwa wamevalia mavazi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona, kinyume cha maelekezo ya Serikali.
“Maafisa hao wawili walionaswa kwenye ile video wamekamatwa. Wamewekwa karantini (kwenye selo tofauti) na watapimwa kama wameathirika na covid-19. Wafanyakazi wote wa mstari wa mbele wanapaswa kuvaa mavazi maalum ya kujikinga,” alisema Ainebyoona.
Kumekuwa na tuhuma za rushwa katika mipaka ya nchi hiyo, ambapo maafisa waliopewa jukumu la kulinda wamedaiwa kupewa hongo na kuruhusu watu kuingia nchini humo kabla ya kupima vizuri vya corona.
Wiki iliyopita, Serikali ya Uganda iliweka masharti magumu zaidi kwa madereva wa malori wanaoingia nchini humo, hii ni baada ya kuwepo taarifa kuwa baadhi ya madereva waliotoka nchi jirani walipimwa na kubainika kuwa na virusi vya corona.