Uongozi wa Klabu ya Young Africans umesema itachukua hatua kali kwa mchezaji Benjamin Asukile, endapo atashindwa kuthibitisha madai yake kuwa kuna baadhi ya viongozi waliowapigia simu baadhi ya wachezaji wa Tanzania Prisons kwa madai ya kutaka kutoa pesa kiasi cha Sh. milioni 40 ili wacheze chini ya kiwango.
Afisa Habari wa Young Africans, Hassan Bumbuli, amesema kuanzia jana Jumatatu (Mei 03) walikuwa kwenye harakati za kuziandikia mamlaka husika kutaka mchezaji huyo ahojiwe na apeleke ushahidi ili hatua zichukuliwe kama kuna baadhi ya watu walihusika na hilo na kama alikuwa anaongea kwa kuichafua klabu ya Young Africans, basi watachukua hatua za kisheria dhidi yake.
“Sisi tumemsikia, ni kauli inayoelekea kuichafua klabu yetu ya Young Africans, anataka kuonyesha kuwa sisi tusingeweza kuishinda timu yao bila kuwatafuta. Yaani timu yao ni bora sana kuliko Young Africans? Wao walifungwa na Ihefu hivi karibuni kwani walihongwa? Young Africans ina unyonge gani wa kushindwa kuifunga Prisons?” Amehoji Bumbuli.
Amesema hawatokubali kulinyamazia jambo hili kwa sababu maana ya mchezaji huyo ni kutaka kuiharibu nembo ya klabu na kuonekana kuwa timu yao haiwezi kuwafunga mpaka watoe kitu fulani.