Mahakama Kuu ya Sudan Kusini jijini Juba imemhukumu kifungo cha miaka miwili kwenda jela mwanaharakati wa kutetea amani na mchumi maarufu nchini humo, Peter Biar Ajak baada ya kukutwa na hatia ya uchochezi na kusababisha ghasia.
Jaji Sumaiya Saleh Abdallah alieleza kwamba Ajak alikiuka vipengele kadhaa vya hati ya kanuni za uhalifu Sudan Kusini na alimhukumu kwa kuvuruga amani kwa sababu alifanya mahojiano na vyombo vya habari vya kigeni.
Wakati huo huo mfanyabiashara maarufu wa Sudan Kusini, Kerbino Wol naye alihukumiwa kifungo cha miaka 13 kwa tuhuma za kuongoza uasi, huku watu wengine wanne wakihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kila mmoja.
Aidha, kwa upande wao wanasheria wa Ajak na Wol wamesema kuwa hawajaridhishwa na hukumu hiyo, hivyo wamedhamiria kukata rufaa kutokana na hukumu hiyo dhidi ya wateja wao.
Ajak ambaye alikuwa akifanya kazi kama mchumi wa benki ya Dunia na alikamatwa Julai mwaka jana baada ya kuwakosoa viongozi wa serikali na upinzani wa Sudan Kusini kwa kushindwa kumaliza miaka mitano ya mgogoro wa kisiasa nchini humo.