Mtoto wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Muhoozi Kainerugaba (48), kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, amechapisha ujumbe akionya kwamba atahitaji wiki mbili pekee na jeshi lake kuiteka Nairobi na kuipindua Serikali ya Ruto.

Hatua ya Muhoozi, ambaye anahudumu kama kamanda wa majeshi ya nchi kavu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF), kuchapisha andiko hilo, inaondoa hali ya kidiplomasia kwa nchi jirani, baada ya kuchapisha mfululizo wa tweets zenye utata kuhusu Kenya.

Awali, alianza kwa kumlaumu Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ambaye anamtaja kama “kaka yake mkubwa”, kwa kutowania muhula wa tatu katika uchaguzi wa Agosti 2022, akiongeza kuwa rais huyo mstaafu angeshinda uchaguzi kirahisi.

Mkuu wa Majeshi ya Nchi Kavu nchini Uganda, Lt-Gen Muhoozi Kainerugaba. Picha na guardian.ng

Amesema, “Tatizo langu pekee na kaka yangu mkubwa ni kwamba hakugombea muhula wa tatu, tungeshinda kirahisi, Kenyatta, ambaye alikabidhi mamlaka kwa Rais William Ruto mnamo Septemba 13, 2022, alifaa kubadilisha katiba ili kusalia mamlakani.”

“Haha! Nawapenda jamaa zangu wa Kenya. Katiba? Utawala wa sheria? Lazima uwe unatania! Kwetu (Uganda), kuna Mapinduzi tu na muda si mrefu mtayafahamu, ninahitaji wiki mbili ili kupindua serikali ya Rais Ruto, haingetuchukua sisi, jeshi langu na mimi, wiki 2 kukamata Nairobi,” alitweet Muhoozi.

Aidha aliendelea kuandika kuwa, “Nina furaha kwamba wanachama wa wilaya yetu nchini Kenya, wamejibu kwa shauku kwenye tweet yangu. Bado ni wiki 2 hadi Nairobi! Baada ya jeshi letu kuteka Nairobi, niishi wapi? Westlands? Riverside?.”

Tweet za Mtoto wa Kwanza wa Museveni, na Kamanda wa Majeshi ya Nchi kavu ya Uganda Peoples Defense Forces (UPDF), Lt. Jenerali Muhoozi Kainerugaba.

Bado haijafahamika mara moja, iwapo Muhoozi ndiye alikuwa anasimamia andiko hilo la akaunti yake ya Twitter au la, na kwa bahati mbaya, Rais Museveni (78), amefaidika mara mbili kutokana na mabadiliko ya katiba ya kuitawala nchini Uganda kwa takriban miongo minne.

Muhoozi ambaye anatajwa kuwa kipenzi cha Museveni na akipigiwa upatu kuwa anaweza kuwa mrithi wa kiti cha Urais nchini humo, pia amemkashifu kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine, akisema kamwe hatatawala Uganda akisema, “Kabobi anapaswa kujua hatutamruhusu kamwe kuwa Rais wa nchi hii!” aliandika Muhoozi.

Miili 42 yagunduliwa katika kaburi la pamoja
Habari kuu kwenye magazeti ya leo Octoba 06, 2022