Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema kuwa shirika la ndege la Tanzania, ATCL limejipanga kikamilifu kuingia katika ushindani wa kibiashara mara baada ya kununua ndege mbili mpya na za kisasa.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili kwa ndege mpya, ambapo amesema kuwa kwasasa huduma za ATCL zimeboreshwa na kuimarika hivyo amewataka wananchi kuzitumia ndege hizo.
”Kwasasa huduma za shirika letu la ndege zimeimalika vya kutosha, na bado tunaongeza jitihada za zingine za kuweza kuwavutia zaidi wateja wetu ambao ni watanzania pamoja na raia wa kigeni kama watalii ili waweze kuzitumia kikamilifu,”amesema Mhandisi Nditiye
Aidha, akizungumzia kuhusu fununu zilizopo kuhusu ATCL kuihujumu Fastjet, amesema kuwa ATCL imejipanga kushindana kibiashara, hivyo kwasasa imeboresha huduma zake kiasi kwamba mashirika mengine ya ndege yamekuwa yakiingiwa na hofu.