Maafisa wa polisi nchini Uganda, wamemkamata mwanamke mmoja aliyekuwa akivuka mpaka wa nchi hiyo kutokea nchini Congo, akiwa amebeba vipodozi haramu alivyokuwa amevifungasha na kuvivalisha kwenye nguo ya mtoto, ambayo ilileta uhalisia wa mtoto mdogo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Bidhaa nchini Uganda, Dickson Kateshumbwa, amesema kuwa bidhaa hizo zilikuwa zimepakiwa vyema katika nguo za mtoto ili kuonekana kwamba ni mtoto, huku Mamlaka ya Mapato nchini Uganda (URA), ikisema kuwa tayari imekwishaitambua mbinu hiyo, hivyo si rahisi kwa msafirishaji yeyote wa vipodozi bandia kupita salama nchini humo.
“Mtoto ghushi alipandishwa gari la kutoka Congo katika kituo cha mpaka wa Mpondwe, na baadae iligundulika mtoto huyo kuwa ni mwanasesele aliyekuwa amesakamiwa vipodozi haramu, baadhi ya walanguzi huendelea kushangaza” alisema Kateshumbwa.
Serikali ya Uganda ilipiga marufuku vipodozi hivyo tangu mwaka 2016, kwa sababu ya kuwa na viwango vya madini ya zebaki na hydroquinone, ambapo utafiti kadhaa umefichua kuwa vina madhara kwa afya, ambapo pia Idara ya Ubora wa Bidhaa (KEBS), iliorodhesha baadhi ya mafuta na bidhaa za urembo ambazo zilikosa, kutimiza masharti ya ubora mnamo Novemba 2019.