Mkazi wa Kijiji cha Mvungwe Wilayani ya Kilindi Mkoani Tanga ameuawa kwa kushambuliwa na ndugu yake baada ya kutokea ugomvi uliotokana na deni la Shilingi 13,000.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Blasius Chatanda, mauaji hayo ya Mahimbo Khatib (40) yalitokea jana saa 1:00 asubuhi katika Kitongoji cha Kwesalaka Kijiji cha Mvungwe wilayani Kilindi baada yaMahimbo kushambuliwa na mdogo wake aliyetajwa kwa jina la Seif Khatib (37)
Watu walioshuhudia tukio hilo walisema ulianza ugomvi baina ya Mahimbo Khatib aliyekuwa akidai Seif Khatib alikuwa anamzungusha kumlipa Sh13,000 alizokuwa akimdai kwa muda mrefu.
Tofauti na ushuhuda wa majirani kuwa ndudugu hao wawili walikuwa na ugomvi, Hussein Daudi ambaye ni Mjomba wa ndugu hao amedai Mahimbo na Seif wana historia ya kusaidiana kwa hali na mali na kwamba hata Mahimbo alishawahi kumkopesha Seif.
“Haiwezekani mwanangu amuue hivi hivi kaka yake ni lazima atakuwa alichezewa akili kwa sababu tangu wakiwa wadogo walikuwa wanapendana,” amesema Hussein, mjomba wa ndugu hao.
Mazishi ya Mahimbo yalifanyika jana saa 9:00 alasiri nyumbani kwao katika Kijiji cha Mavungwe wilayani Kilindi na Jeshi la polisi linamsaka Seif ili afikishwe kwenye vyombo vya Sheria kujibu shtaka la mauaji.