Maelfu ya watu nchini Australia wamekimbilia ufuo wa bahari kujinusuru na moto wa nyikani ambao unaelekea maeneo ya pwani.
Wakazi wa Mallacoota wameiambia BBC kuwa moto huo ni “kisa cha kuogofya” huku wakisimulia jinsi walivyoona anga ilivyobadilika rangi nyekundu wakiwa ndani ya boti.
Maafisa wamethibitisha kuwa watu wawili wamefariki kutokana na moto huo katika mji wa New South Wales (NSW), hadi kufikia sasa vifo 12 vimehusishwa na janga hilo la moto.
Miili ya waathiriwa wa hivi punde ambayo inaaminiwa kuwa ya baba na mwanawe wa kiume ilipatikana katika mji wa Corbargo eneo la NSW, ambalo lilikumbwa na moto siku ya Jumanne.
Gavana wa jimbo la Victoria Daniel Andrews amesema meli huenda zikatumwa kuwapelekea wahanga wa moto huo chakula, maji na nguvu za umeme katika maeneo hayo.
Mamlaka zilitoa wito kwa watu wa eneo hilo wengi wao watalii kutoondoka lakini ilipofika Jumatatu hali ilikuwa mbaya na hatari kufanya shughuli ya kuwahamisha.
Moto wa nyikani katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo umetokana na ongezeko la viwango vya joto, upepo mkali na radi ya wakati wa ukame