Hali ya Rais wa Simba Evance Aveva imeelezwa kuwa siyo nzuri baada ya kuugua akiwa Mahabusu Keko jijini Dar es salaam kisha kukimbizwa katika Hospitali ya Temeke jana.

Taratibu zinafanywa kumuhamishia Hospitali ya Muhimbili.

Aveva na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, wanakabiliwa na tuhuma za kughushi nyaraka za klabu hiyo na kutakatisha dola 300,000 (zaidi ya Sh 650 milioni) na wamekuwa rumande tangu Juni 29, mwaka jana.

Taarifa zinaeleza, familia na marafiki wa Aveva walikuwa na mazungumzo na Jeshi la Magereza kwa ajili ya kuomba uhamisho wa kumpeleka hospitali kutokana na aina ya matibabu anayoyapata Hospitali ya Temeke.

Mtoa taarifa huyo alisema, rais huyo anahitaji kupatiwa matibabu mazuri yatakayoendana na ugonjwa ambao ni siri ili apate nafuu arejee katika hali yake ya kawaida.

“Aveva jana (juzi) asubuhi hali yake ilibadilika na kusababisha akimbizwe kwenye Hospitali ya Temeke kwa ajili ya kupata matibabu ya afya yake.

“Lakini wakati akiendelea na matibabu Temeke, baadhi ya ndugu na marafiki wamejaribu kuliomba Jeshi la Magereza kwa ajili ya kupata ruhusa ya kumhamishia Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya kupata matibabu mazuri,” alisema mtoa taarifa huyo.

Chama kuzikwa kesho Jumanne, Young Africans waomboleza
Gigy Money atoa chozi Basata