Mmiliki wa klabu ya Chelsea Roman Abramovich, anafirikia kumuongezea nguvu meneja wa klabu hiyo Frank Lampard, kwa kumuajiri Avraham “Avram” Grant, ambaye aliwahi kupita klabuni hapo kama mkurugenzi wa ufundi na mkuu wa benchi la ufundi.
Abramovich anaamini endapo atafanikiwa kurudisha Grant klabuni hapo, atatoa msaada mkubwa kwa Lampard na benchi lake la ufundi katika kuhakikisha kikosi cha Chelsea kinarudisha makali yake kama ilivyokua mwanzoni mwa msimu huu.
Chelsea FC imeshinda mchezo mmoja kati ya michezo sita ya Ligi Kuu England EPL, hali ambayo imeifanya klabu hiyo kushika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi hiyo pendwa duniani.
Hata hivyo Avram raia Israel anaamini kwa uwezo wake, anafaa kuwa meneja wa timu na sio kufanya kazi nyuma ya pazia kama inavyofikiriwa na mmiliki wa Chelsea, hii inamaanisha endapo atatua Stamford Bridge, itakuwa ni kama anapita tu na sio kufanya kazi kwa muda mrefu.
Avram aliiongoza Chelsea kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi ya England, Ligi ya Mabingwa na Kombe la FA msimu wa 2007/08.