Wakati kikosi cha timu ya Azam FC kikianza kujifua jijini Sousse nchini Tunisia, tayari kwa msimu ujao wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa, mambo yamezidi kuwa moto ambapo kikosi hicho kitacheza mechi tano za kirafiki.
Azam FC iliondoka nchini mwishoni mwa juma lililopita kuelekea Tunisia kuweka kambi ya majuma matatu kujiandaa na msimu mpya 2023/24.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Thabiti Zakaría Zaka za Kazi, amesema kikosi chao kimefika salama nchini Tunisia na kocha wao, Youssoph Dabo amehitaji mechi tano za kirafiki.
“Mwalimu wetu Dabo anahitaji mechi tano za kirafiki ni kuhakikisha anawasoma vema wachezaji wake na kuwapa mifumo bora ili wakirejea kuwa na kikosi imara kitakachokuwa tishio kwa wapinzani,” amesema.
Zaka amesema kocha huyo anataka timu hiyo icheze mechi hizo kuweza kuwasoma vyema wachezaji wake.
Hata hivyo, Afisa huyo amesema wapo katika hatua za mwisho kusaka timu ambazo wataenda kucheza nazo na baadae wataziweka wazi.
Zaka amesema kocha Dabo anaamini atatumia muda huo kujenga kikosi chake na kuwapa mbinu wachezaji wake.
Hadi sasa Azam imesajili wachezaji wanne ambao ni Mtanzania Feisal Salum, Mgambia Djibril Sillah, Alassane Diao na Cheikh Tidiane Sidibe wote kutoka Senegal.