Mabingwa wa kombe la shirikisho Tanzania bara (ASFC) Azam FC, wanaamini muda si mrefu wataingia kwenye orodha ya vilabu vinavyoongoza kuwa na wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii barani Afrika.
Azam FC wameonyesha dhamira hiyo, baada ya kampuni kinara ya Afrika Kusini inayojihusisha na utafiti wa kidigitali wa michezo katika mitandao ya kijamii Digital Sports Africa, kutoa orodha ya vilabu kumi vinavyoongoza kuwa na wafuasi wengi kwa mwezi Aprili, juzi jumanne.
Kwa mujibu wa mtandao wa Digital Sports Africa, wafuasi hao wametoka katika mitandao ya Instagram, Facebook, Twitter, YouTube, TikTok na linkedin, ambapo klabu ya Al Ahly ya nchini Misri inaongoza ikiwa na wafuasi milioni 27, ikifuatiwa na Zamalek SC yenye wafuasi milioni 12 na Raja Club Athletics ya Morocco ikishika nafasi ya tatu kwa wafuasi milioni 6.
Mabingwa wa soka Tanzania bara Simba SC, ndiyo klabu pekee kutoka ukanda wa Afrika mashariki na kati kuwemo katika orodha ya vilabu 10 bora vinavyoongoza kwa wafuasi kupitia mitandao ya kijamii (wafuasi 2M).
Klabu ya Azam FC inakamata nafasi ya 13 katika orodha hiyo ikiwa na wafuasi takribani wafuasi milioni 1 na klabu ya Yanga 957,000.
Mkuu wa idara ya habari na mawasilino Azam FC Thabit Zakaria, ameandika kwenye ukurasa wake wa facebook kuwa, wanaamini klabu yao ipo kwenye nafasi nzuri ya kupanda na kuingia kwenye kumi bora miezi michache ijayo.
“Azam FC imevipita vilabu vikubwa vya Afrika kama Esperance na Etoile du Sahel za Tunisia, Hearts of Oak na Asante Kotoko za Ghana, Wydad Casablanca ya Morocco, TP Mazembe ya DRC na Yanga ya Tanzania.”
“Kwa timu iliyoanza kushiriki ligi kuu msimu wa 2008/09, hii ni dalili njema sana ya mwangaza huko mbele kwamba klabu yetu inafuatiliwa ndani na nje ya nchi yetu.”
“Miaka 10 ya kwanza kwenye ligi imekuwa ya kujifunza na kujiimarisha, 10 inafuata itakuwa ya kutawala na kushika hatamu.” Ameandika Thabit Zakaria.