Uongozi wa Azam FC umetoa ufafanuzi wa kuachana na Kiungo kutoka Visiwani Zanzibar Mudathir Yahya, baada ya kuthibitisha taarifa hizo jana Jumatatu (Agosti Mosi).
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC Thabit Zakaria ‘Zakazakazi’ amesema Uongozi umefanya maamuzi ya kuachana na Mudathir, baada ya kujiridhisha kuwa kiungo huyo hakutaka kuendelea kufanya kazi ndani ya klabu hiyo katika kipindi hiki.
Amesema kabla ya kutangazwa kwa maamuzi ya kuachwa, Uongozi ulimpa Mkataba mpya Mudathir, baada ya Mkataba wa awali kufikia kikomo tangu Juni 30, lakini kiungo huyo alishindwa kuusaini kwa wakati, licha ya kusubiriwa kwa zaidi ya mwezi mmoja.
“Alipewa Mkataba mpya tangu mwezi Juni wakati Mkataba wake wa awali ukiwa unaendelea kufanya kazi, lakini hadi mwezi Julai unamalizika Mudathir hakusaini Mkataba mpya aliokuwa amepewa na Uongozi”
“Jambo la Kwanza kabla ya kutangazwa kuachwa, Uongozi uliitoa namba yake ya Jezi (27) kwa mchezaji Maliku Ndowe, kwa sababu tuliyekua tunamsubiri hakuonesha nia ya kutaka kuendelea na sisi.”
“Wachezaji wengine tulianachana nao ni Charles Zulu na Paul Katema, tayari namba walizokua wanazitumia katika jezi zao tumeshazitoa kwa wachezaji wetu wengine tulionao hapo Kambini Misri.” amesema Thabit Zakaria.
Katika hatua nyingine Thabit amesema kikosi cha Azam FC kesho Jumatano (Agosti 03) kitacheza mchezo wa pili wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi Suez SC.
Katika mchezo wa kwanza Azam FC ilipoteza kwa 1-0 dhidi ya Wadi Degla.