Mabingwa wa kombe la shirikisho Tanzania bara (ASFC) Azam FC wamesema wapo tayari kurejea kwa ligi kuu ya soka Tanzania bara, licha ya kukabiliwa na tatizo la benchi la ufundi.
Mkuu wa idara ya habari na mawasilino wa Azam FC Thabit Zakaria amesema kocha mkuu Aristica Cioaba na msaidizi wake hawapo nchini kwa sasa, na wanahofia huenda ikawachukua muda kurejea kwenye majukumu yao, kutokana na taratibu zilizotangazwa na TFF pamoja na Bodi Ya Ligi.
“Tupo tayari kupambana na tumefurahishwa na kauli iliyotolewa na Rais Magufuli, sisi ni timu ya mpira na tupo tayari kupambana,”
“Kwa upande mwingine tupo kwenye wakati mgumu sana, makocha wetu wapo nje ya nchi, kocha mkuu yupo Romania na kocha msaidizi yupo Burundi, kwa hiyo kama ligi itarudi maana yake tutarudi kwenye ligi bila makocha.”
“Inafahamika wazi kuwa serikali nyingi zimefunga mipaka(viwanja vya ndege), ndege hazisafiri, zimefuta safari, kwa hiyo hawa watu hawawezi kurudi kwa wakati.”
“Pia tuna wachezaji saba wa kigeni ambao wapo nje, wachezaji watatu wapo Ghana, watatu wapo Zimbabwe na mmoja yupo Uganda, kwa hiyo ni mazingira magumu kwetu, hivyo tutakua na wakati mgumu, japo tunaweza kuvumilia kwa wachezaji, kwa sababu tunaweza kuwatumia hawa wa nyumbani.” Alisema Thabit Zakaria
Katika hatua nyingine Zakaria amezungumzia suala la ligi kuchezwa bila mashabiki pamoja na kanuni ya michezo ya ligi hiyo kuchezwa nyumbani na ugenini, kama afisa mtendaji wa bodi ya ligi alipotoa taarifa ya uwezekano wa kurejea kwa ligi kuu mwanzoni mwa kwezi Juni.
“Kucheza Ligi bila mashabiki hiyo ni dharura ni kama mko vitani hauchagui silaha iliyo karibu ndio unayotumia, kama tukisema kwenye vita hii silaha ni kucheza bila mashabiki wacha iwe hivyo”
“Mashabiki wakae nyumbani watapata taarifa kupitia vyombo vya habari lakini mimi ningependa ichezwe iwe kwa kituo rasmi sio ichezwe nchi nzima kama ilivyokuwa timu mnasafiri mnakwenda huku nadhani hiyo itakuwa hatari zaidi.
“Ingeweza kucheza katika eneo moja tu huku tukiangalia namna ambayo tutaokoa wanamichezo wetu na watu wote wanaohusika na Ligi”- Thabit Zacharia (Mkuu Wa Idata Ya Habari Na Mawasiliano – Azam FC.